Abstract
Mhusika ni kigezo msingi kinachomfanikisha mtunzi wa kazi ya fasihi katika kuwasilisha ujumbe wake. Umuhimu wa mhusika katika kazi za kifasihi si suala la kupuuzwa na mtafiti yeyote. Watafiti mbalimbali wakiwa wametafitia kijenzi cha mhusika katika fasihi ya Kiswahili suala la uainishaji wa mhusika kwa msingi wa utendakazi katika jamii halijashughulikiwa kwa ukamilifu. Utafiti huu ulikuwa muhimu kwa kuwa mtafiti alichanganua uainishaji wa mhusika kwa msingi wa utendakazi wa upelelezi katika riwaya teule za Kiswahili ambazo ni: Simu ya kifo (1965), Kisima cha Giningi (1968) na Najiskia Kuua Tena (1984). Mtafiti aliongozwa na nadharia ya uhalisia wa kisasa. Mtafiti alitumia muundo wa kimaelezo. Kundi lengwa la utafiti lilikuwa riwaya za Kiswahili ambazo zimesawiri masuala ya kiupelelezi. Sampuli kimakusudi ya riwaya tatu za kiupelelezi ambazo ni: Simu ya Kifo (1965), Kisima cha Giningi (1968) na Najiskia Kuua Tena (1984) ziliteuliwa. Data ya utafiti ilikusanywa kwa kusoma riwaya teule kwa kunukuu hoja muhimu zilizowezesha kujibu maswali ya utafiti. Data ilichanganuliwa kwa kuainisha mhusika mpelelezi kwa kuongozwa na lengo la utafiti. Utafiti ulibainisha kuwa mhusika katika kazi ya kifasihi anaweza kuainishwa katika mikabala mbalimbali kutegemea utendakazi wake katika kazi ya kifasihi. Waandishi wa riwaya teule wamedhihirisha hivyo kupitia ujenzi wa mhusika anayefanya kazi ya upelelezi. Utafiti huu ni muhimu kwa kuwa unaarifu watafiti wa kifasihi kuhusu umuhimu wa mhusika katika kuweka wazi masuala yanayoendelea katika jamii pana pamoja na kuwa msingi wa tafiti za baadaye kuhusiana na fasihi andishi zinazohusu masuala ya kifasihi andishi ambayo yamekuwepo lakini bado kutafitiwa.